Ilani ya Faragha ya Google Payments
Ilibadilishwa mara ya mwisho tarehe 18 Novemba 2024
Sera ya Faragha ya Google inaeleza jinsi tunavyoshughulikia taarifa binafsi unapotumia bidhaa na huduma za Google. Ikiwa una umri wa chini ya miaka 18, unaweza kupata nyenzo za ziada katika Mwongozo wa Google wa Faragha kwa Vijana.
Huduma ya Google Payments inatolewa kwa wamiliki wa Akaunti za Google na unaitumia kwa mujibu wa Sera ya Faragha ya Google. Pia, Ilani hii ya Faragha inaeleza kuhusu desturi za faragha za Google zinazotumika kwenye Google Payments.
Matumizi yako ya Google Payments yanasimamiwa na Sheria na Masharti ya Google Payments, ambayo yanaeleza kwa kina zaidi kuhusu huduma zilizojumuishwa katika Ilani hii ya Faragha. Maneno yaliyoandikwa kwa herufi kubwa ambayo hayajafafanuliwa katika Ilani hii ya Faragha yamefasiliwa katika Sheria na Masharti ya Google Payments.
Ilani ya Faragha ya Google Payments inatumika kwenye huduma zinazotolewa na Google LLC au kampuni inazomiliki kikamilifu, ikiwa ni pamoja na Google Payment Corp. ('GPC'). Soma Sheria na Masharti ya Google Payments yanayopatikana katika huduma ili ufahamu kampuni tanzu inayotoa huduma husika.
- Kwa watumiaji wanaoishi Brazili, mdhibiti wa data yao ni Google LLC na kadiri inavyotakiwa na sheria za Brazili, mdhibiti anaweza kuwa Google Brasil Pagamentos Ltda
- Kwa watumiaji (isipokuwa wanaouza kwenye soko la Google) wanaoishi katika nchi washirika kwenye Makubaliano ya Kiuchumi ya Ulaya (isipokuwa Uingereza), mdhibiti wa data yao ni Google Ireland Limited
- Kwa watumiaji wanaoishi katika nchi washirika kwenye Makubaliano ya Kiuchumi ya Ulaya, isipokuwa Uingereza na wanauza kwenye soko la Google, mdhibiti wa data yao ni Google Payment Ireland Limited
- Kwa watumiaji (isipokuwa wanaouza kwenye soko la Google) wanaoishi Uingereza, mdhibiti wa data yao ni Google LLC
- Kwa watumiaji wanaoishi Uingereza na wanauza kwenye soko la Google, mdhibiti wa data yao ni Google Payment Limited
Taarifa tunazokusanya
Kando na taarifa zilizoorodheshwa katika Sera ya Faragha ya Google, tunaweza pia kukusanya taarifa zifuatazo:
Taarifa za usajili
Unapojisajili kwenye Google Payments, unaweka taarifa za malipo kwenye Google zinazohusishwa na Akaunti yako ya Google. Kulingana na huduma za Google Payments unazotumia, huenda ukaombwa uweke taarifa zingine, kando na taarifa zilizoorodheshwa katika Sera ya Faragha ya Google, kama vile:
- Namba ya kadi ya mikopo au ya malipo na tarehe ya mwisho ya kutumia kadi hiyo
- Namba ya akaunti ya benki na tarehe ya mwisho ya kuitumia
- Anwani
- Namba ya simu
- Tarehe ya kuzaliwa
- Namba ya bima ya kitaifa au namba ya utambulisho wa mlipakodi (au namba za vitambulisho vingine vinavyotolewa na serikali)
- Kwa wauzaji au biashara, aina ya biashara yako na maelezo fulani kuhusu kiasi cha mauzo au miamala yako
Wakati mwingine, tunaweza pia kukuomba ututumie taarifa za ziada au ujibu maswali ya ziada ili tuweze kuthibitisha taarifa au utambulisho wako. Hatimaye, ukisajili akaunti ya bili ya mtoa huduma au ya kampuni ya simu, tutakuomba utupatie maelezo fulani kuhusu akaunti unayotumia ya mtoa huduma au kampuni ya simu.
Taarifa zako za usajili huhifadhiwa zikiwa zimehusishwa na Akaunti yako ya Google na usajili wako wa njia ya kulipa utahifadhiwa kwenye seva za Google. Aina fulani za data zinaweza pia kuhifadhiwa kwenye kifaa chako cha mkononi.
Taarifa tunazopata kutoka kwa washirika wengine
Tunaweza kupata taarifa zinazokuhusu kutoka kwa washirika wengine, ikiwa ni pamoja na huduma za uthibitishaji za washirika wengine. Taarifa hizi ni pamoja na:
- Taarifa zinazotokana na miamala ya Google Payments katika maeneo ya wauzaji
- Maelezo kuhusu jinsi unavyotumia njia za kulipa na akaunti zako zinazotolewa na washirika wengine, ambazo umeunganisha na Google Payments
- Utambulisho wa taasisi ya kifedha au kampuni iliyotoa kadi yako
- Maelezo kuhusu vipengele na manufaa yanayohusishwa na njia yako ya kulipa
- Maelezo kuhusu ufikiaji wa masalio yaliyo katika taarifa zako za malipo kwenye Google
- Maelezo kutoka kwa mtoa huduma au kampuni ya simu yanayohusiana na malipo kupitia mtoa huduma au kampuni hiyo ya simu
- Ripoti za watumiaji, kulingana na fasili ya neno 'ripoti za watumiaji' kwa mujibu wa Sheria ya Marekani ya Utoaji wa Taarifa za Kifedha kwa Haki
- Maelezo kuhusu miamala yako na washirika wengine (kama vile wauzaji na watoa huduma za malipo), yatakayotumiwa kubuni mifumo ya kudhibiti hatari za ulaghai na kuwapatia washirika wengine alama za hatari za ulaghai na huduma nyingine za kuzuia ulaghai
Pia, ikiwa wewe ni muuzaji, tunaweza kukusanya taarifa kukuhusu wewe na biashara yako kutoka kwa taasisi ya mikopo au huduma ya maelezo ya biashara.
Maelezo ya miamala
Unapotumia Google Payments kufanya muamala, tunaweza kukusanya maelezo kuhusu muamala huo, ikiwa ni pamoja na:
- Tarehe, saa na kiasi cha muamala
- Mahali muuzaji alipo na maelezo kumhusu
- Maelezo yaliyotolewa na muuzaji wa bidhaa au huduma ulizonunua
- Picha yoyote unayochagua kuhusisha na muamala
- Majina na anwani za barua pepe za muuzaji na mnunuzi (au mtumaji na mpokeaji)
- Aina ya njia ya kulipa uliyotumia
- Maelezo yako kuhusu sababu za kufanya muamala na ofa inayohusishwa na muamala huo, ikiwa ipo
Jinsi tunavyotumia taarifa tunazokusanya
Mbali na matumizi yaliyoorodheshwa katika Sera ya Faragha ya Google, tunatumia taarifa unazotupatia sisi, Google Payment Corp. (GPC) au kampuni tanzu nyingine tunazomiliki, pamoja na taarifa zako kutoka kwa washirika wengine, ili:
- Kukupatia Google Payments kwa madhumuni ya huduma kwa wateja
- Kulinda haki, mali au usalama wa Google, watumiaji wetu au umma, ikiwemo kukulinda dhidi ya ulaghai, wizi wa data binafsi au matendo mengine yasiyofaa
- Kuwasaidia washirika wengine kukupatia bidhaa au huduma unazowaomba
- Kukagua taarifa zako za malipo kwenye Google ili kubaini iwapo bado unatimiza sheria na masharti ya huduma
- Kufanya uamuzi kuhusu miamala yako ya baadaye kwenye Google Payments
- Kubuni na kufundisha mifumo ya kudhibiti hatari za ulaghai kwa kutumia taarifa zako za zamani na za sasa na kutoa tathmini na alama za hatari za ulaghai zinazotumwa kwa washirika wengine ili wazitumie tu kwa madhumuni ya kuzuia ulaghai au matumizi mabaya
- Kukupatia maelezo kuhusu vipengele na manufaa ya njia yako ya kulipa ili kukusaidia utambue vizuri zaidi njia yako ya kulipa unapotumia Google Payments
- Kukidhi mahitaji mengine halali ya kibiashara yanayohusiana na miamala unayoanzisha kwenye Google Payments
Tunaweza kuhifadhi taarifa unazotupatia kwa kipindi unachotumia Google Payments na kwa kipindi cha ziada inapohitajika ili kutii wajibu wetu wa kisheria na kikanuni.
Taarifa tunazoruhusu zifikiwe
Tutaruhusu tu taarifa zako binafsi zifikiwe na kampuni au watu wengine binafsi nje ya Google katika hali zifuatazo:
- Kama inavyoruhusiwa kwa mujibu wa Sera ya Faragha ya Google
- Kama inavyoruhusiwa na sheria
- Inapohitajika ili kuchakata muamala wako na kudumisha akaunti yako, ikiwa ni pamoja na kuimarisha usalama, kulinda akaunti yako dhidi ya ulaghai na kwa madhumuni mengine ya kawaida ya kibiashara
- Kukamilisha usajili ulioomba wa huduma inayotolewa na mshirika mwingine
- Kumfahamisha muuzaji mwingine, unayetembelea tovuti au programu yake, iwapo una taarifa za malipo kwenye Google unazoweza kutumia kumlipa muuzaji huyo kupitia tovuti au programu yake. Unaweza kuchagua kuzima mipangilio hii
- Kutuma alama za hatari za ulaghai na tathmini nyingine za ulaghai kwa washirika wengine wanaotumia huduma za kuzuia ulaghai na alama ya hatari ya ulaghai kutoka Google, ili kulinda miamala yako na washirika wengine dhidi ya ulaghai na matumizi mabaya
- Ili kusaidia kuhakikisha kuwa njia yako ya kulipa ni salama na sahihi na kukupatia maelezo yanayofaa kuhusu vipengele na manufaa ya njia yako ya kulipa, tunaweza kuruhusu taarifa zako binafsi zifikiwe na kampuni iliyokupa njia ya kulipa, mtandao wa malipo, watoa huduma za kuchakata malipo na washirika wao
Mifano ya wakati tunaweza kuruhusu taarifa zifikiwe:
- Unapofanya ununuzi au muamala ukitumia Google Payments, tutaruhusu taarifa zako fulani binafsi zifikiwe na kampuni au mtu binafsi unayenunua kwake au kufanya naye biashara. Hii ni pamoja na kuruhusu taarifa zako binafsi zifikiwe na msanidi programu unayenunua kwake ukitumia Google Payments kwenye Google Play
- Unapofanya ununuzi kupitia tovuti au programu ukitumia Google Pay, huenda tukaruhusu ufikiaji wa msimbo wa eneo au msimbo wako wa posta na maelezo kuhusu njia yako ya kulipa ili muuzaji aweze kukokotoa kodi, ada za usafirishaji na maelezo mengine yanayohusiana na gharama ya oda yako (kama vile gharama za kuletewa bidhaa na maelezo mengine ya bei) na kubaini iwapo muuzaji anaweza kukubali njia hiyo ya kulipa kutoka kwako pamoja na manufaa au vizuizi vya njia fulani za kulipa kwenye ununuzi wako
- Unapoweka njia ya kulipa ya mtoa huduma mwingine katika taarifa zako za malipo kwenye Google, tunaweza kubadilishana taarifa fulani binafsi na mtoa huduma huyo wa malipo ili sote tuweze kukupatia huduma husika. Taarifa hizo zinaweza kujumuisha jina, picha ya wasifu, anwani ya barua pepe, anwani ya Itifaki ya wavuti (IP), anwani ya kutuma bili, namba ya simu, maelezo ya kifaa, data ya mahali ulipo na maelezo kuhusu shughuli zako za Akaunti ya Google
- Unapotembelea programu au tovuti ya muuzaji mshiriki, muuzaji huyo anaweza kuangalia iwapo una taarifa za malipo kwenye Google zilizo na njia ya kulipa inayoweza kutumika kufanya ununuzi kupitia tovuti au programu ya muuzaji. Hatua hii husaidia kuchuja vipengele visivyotumika ili usivione kwenye tovuti au programu
- Unapofanya muamala na mshirika mwingine (kama vile wauzaji na watoa huduma za malipo), tunaweza kutuma alama za hatari za ulaghai na tathmini nyingine za ulaghai zinazohusiana na muamala wako wa malipo kwa washirika hawa wengine, ili wazitumie tu kwa madhumuni ya kuzuia ulaghai au matumizi mabaya
Taarifa tunazokusanya, zikiwemo taarifa tunazopata kutoka kwa washirika wengine, zinaweza kufikiwa na washirika wetu, yaani kampuni zinazomilikiwa na kudhibitiwa na Google LLC. Washirika wetu, ambao wanaweza kuwa asasi za kifedha na zisizo za kifedha, watatumia taarifa hizo kwa madhumuni yaliyobainishwa katika Ilani hii ya Faragha pamoja na Sera ya Faragha ya Google, ikiwemo kwa madhumuni yao ya kawaida ya kibiashara.
Tunakupatia haki ya kutoruhusu ufikiaji wa taarifa kati ya GPC na washirika wake, panapofaa. Hasa, unaweza kuchagua kutoruhusu:
- Ufikiaji wa maelezo kuhusu uwezo wako wa kukopesheka, kati ya GPC na washirika wake kwa madhumuni ya shughuli zao za kawaida za kibiashara; na/au
- Washirika wetu kukutangazia bidhaa au huduma zao kulingana na taarifa zako binafsi tunazokusanya na kuwaruhusu wafikie. Taarifa hizi ni pamoja na historia ya shughuli zako za akaunti kwenye huduma zetu
Unaweza pia kuchagua kutoruhusu Google LLC au washirika wake wasimfahamishe muuzaji mwingine, unayetembelea tovuti au programu yake, iwapo una taarifa za malipo kwenye Google unazoweza kutumia kumlipa muuzaji huyo kupitia tovuti au programu yake.
Ukichagua kutoruhusu ufikiaji wa taarifa zako, chaguo lako litatumika hadi utakapotuambia tulibadilishe.
Ikiwa hungependa turuhusu ufikiaji wa taarifa binafsi kuhusu uwezo wako wa kukopesheka, kati ya GPC na washirika wake; au ikiwa hungependa washirika wetu wakutangazie bidhaa na huduma zao wakitumia taarifa zako binafsi tulizokusanya na kuwaruhusu wafikie; au ikiwa hungependa Google LLC au washirika wake wamfahamishe muuzaji mwingine, ambaye unatembelea tovuti au programu yake, iwapo una taarifa za malipo kwenye Google, tafadhali weka mapendeleo yako kwa kuingia katika akaunti yako kisha uende kwenye ukurasa wako wa mipangilio ya faragha ya Google Payments ili usasishe mapendeleo yako ya faragha.
Hatutaruhusu taarifa zako binafsi zifikiwe na mtu yeyote nje ya GPC au na washirika wetu isipokuwa katika hali zilizobainishwa kwenye Ilani hii ya Faragha au Sera ya Faragha ya Google. Google Payments ni bidhaa inayotolewa kwa wamiliki wa Akaunti za Google. Data unayotuma kwa Google LLC kwa madhumuni ya kufungua Akaunti ya Google haiathiriwi na masharti ya kutoruhusu ufikiaji wa taarifa, ambayo yametajwa kwenye Ilani hii ya Faragha.
Kulinda taarifa zako
Ili upate maelezo zaidi kuhusu mbinu zetu za usalama, tafadhali soma Sera ya Faragha ya Google.
Usalama wa taarifa zako za malipo kwenye Google unategemea jinsi utakavyoweka siri manenosiri ya akaunti, PIN na maelezo mengine ya kufikia Huduma:
- Ukiruhusu taarifa za Akaunti yako ya Google zifikiwe na mshirika mwingine, atafikia taarifa zako za malipo kwenye Google pamoja na taarifa zako binafsi
- Ni wajibu wako kudhibiti ufikiaji wa kifaa chako cha mkononi na programu ya Google Payments kwenye kifaa chako, ikiwa ni pamoja na kuweka siri manenosiri na/au PIN yako na kutomruhusu mtu yeyote kuifikia
- Pia, ni wajibu wako kuifahamisha Google au mshirika husika ikiwa unaamini kwamba usalama wa taarifa zilizo katika programu ya Google Payments umeathiriwa
Taarifa zozote unazotoa moja kwa moja kwa muuzaji, kwenye tovuti au programu ya mshirika mwingine hazijumuishwi katika Ilani hii ya Faragha. Hatuwajibikii desturi za faragha au usalama za wauzaji au washirika wengine unaoshiriki nao taarifa yako binafsi moja kwa moja. Tunakuhimiza usome sera za faragha za washirika wengine wowote unaochagua kuruhusu wafikie taarifa zako binafsi moja kwa moja.
© 2024 Google – Google Home Sheria na Masharti ya Google Ilani za Faragha za Awali